John 20

Kufufuka Kwa Isa

(Mathayo 28:1-8; Marko 16:1-8; Luka 24:1-12)

1 aAlfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa kungali giza bado, Maria Magdalene alikwenda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio. 2 bHivyo akaja akikimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Isa alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!”

3 cPetro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara kuelekea kaburini. 4Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5 dAlipofika, akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani mle ndani, lakini hakuingia. 6Ndipo Simoni Petro akaja, akimfuata nyuma akaenda moja kwa moja hadi ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini 7 ena kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Isa. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa mahali pa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda. 8 fKisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini naye akaingia ndani, akaona, akaamini, 9 g(kwa kuwa mpaka wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Isa afufuke kutoka kwa wafu).

10Kisha hao wanafunzi wakaondoka wakarudi nyumbani kwao.

Isa Anamtokea Maria Magdalene

(Mathayo 28:9-10; Marko 16:9-11)

11 hLakini Maria Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama, kuchungulia mle kaburini, 12 inaye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Isa ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.

13 jWakamuuliza Maria, “Mwanamke, mbona unalia?”

Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu na sijui walikomweka.”
14 kBaada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Isa amesimama, lakini hakumtambua.

15 lIsa akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?”

Maria akidhani ya kuwa aliyekuwa anaongea naye ni mtunza bustani, kwa hiyo akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nionyeshe ulikomweka, nami nitamchukua.”

16 mIsa akamwita, “Maria!”

Ndipo Maria akamgeukia Isa na kusema naye kwa Kiebrania, “Rabboni!” (Maana yake Mwalimu).

17 nIsa akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”

18 oKwa hiyo Maria Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Isa, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Isa alikuwa amemweleza mambo hayo yote.

Isa Awatokea Wanafunzi Wake

(Mathayo 28:16-20; Marko 16:14-18; Luka 24:36-49)

19Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi. Naye Isa aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” 20 pBaada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana.

21 qIsa akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22 rNaye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 sMkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa, na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”

Isa Anamtokea Tomaso

24 tLakini Tomaso, aliyeitwa Didimasi, yaani Pacha, mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Isa alipokuja. 25 uHivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.”

Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”

26 vBaada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Isa akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.” 27 wKisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”

28 xTomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

29 yIsa akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”

Kusudi La Kitabu Hiki

30 zIsa alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31 aaLakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Isa ndiye Al-Masihi,
Al-Masihi maana yake ni Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.
Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.
Copyright information for SwhKC